tangazo

Thursday, May 5, 2011

Serikali na mkakati wa kutokomeza maleria nchini

*Waziri Mponda ataka jamii iongeze kasi ya vita

Na Rabia Bakari

UGONJWA wa maleria ni moja ya tisho kubwa kwa watanzania ukiachilia mbali UKIMWI,Kifua Kikuu (TB) na homa ya matumbo.Serikali na kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) kwa kushirikiana na wadau wakiwemo wahisani wamekuwa na juhudi kubwa
kuhakikisha ugonjwa wa malaria unapungua na hatimaye kwisha kabisa.
 
Japo ugonjwa huo unaonekana kuwa tishio kwa miaka mingi lakini kwa kiasi kikubwa mikakati iliyopo kupambana na malaria imesaidia kushusha kiwango cha maambukizi.

Taarifa za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaonesha kuwa ugonjwa huo unaongoza kwa mahudhurio ya Wagonjwa wa Nje (OPD) katika vituo vya afya na wale wanaolazwa katika hospitali nyingi hapa nchini.
  
Waziri wa Afya, Dkt. Haji Mpanda, anasema pia ugonjwa huo unaongoza kwa vifo vyote vinavyotokea katika vituo vya huduma ya tiba nchini.

Anasema taarifa ya utafiti ya ugonjwa wa malaria na UKIMWI ya mwaka 2007/2008, inaonesha kuwa asilimia 18 ya watoto wenye umri kati ya miezi 6 hadi miaka 5 waliofanyiwa kipimo cha malaria Tanzania Bara walionekana kuwa na vimelea vya ugonjwa huo na asilimia 1 kwa Tanzania visiwani.

"Tathmini hiyo imeonesha kuwa mikoa ya Kanda ya Ziwa,  Kanda ya Kusini, na Mikoa ya Kanda ya Magharibi ina maambukizi ya malaria kati ya asilimia 21 hadi 40, na maeneo ya mikoa ya kanda nyingine zilizosalia yana maambukizi yasiozidi asilimia 14.

Takwimu toka katika Vituo vya kutolea Huduma za Afya zinaonesha idadi ya vifo kwa watoto chini ya miaka mitano kwa kipindi cha kati ya  mwaka 2003 hadi 2007.

Mwaka 2003 kulikuwa na vifo 7,907; Mwaka 2004 vifo 8,853; Mwaka 2006 vifo 8,297 na Mwaka 2007 vifo 6,676,"anaongeza Waziri Mpanda.

Anafafanua kuwa hiyo ni idadi ya vifo vinavyotokea kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pekee na haijumuishi vifo vinavyotokea nyumbani.

"Ni dhahiri kwamba idadi halisi ya vifo vinavyotokana na malaria ni kubwa zaidi na inakadiriwa kuwa vifo  80,000 hutokea kila mwaka,"anafafanua.

Ugonjwa wa malaria umekuwa na athari kubwa hasa kiuchumi kwa kupunguza nguvu kazi ya taifa ambapo pia serikali imekuwa ikipoteza kiasi cha asilimia 3.4 ya pato la kitaifa kila mwaka kutokana na ugonjwa huo.

Waziri Mpanda anasema changamoto kubwa kwa jamii ni kutafakari kwa makini kuhusu juhudi gani zaidi zifanyike kupambana na ugonjwa huo.

"Hatuna sababu malaria kuendelea kututesa na kudhoofisha maendeleo ya nchi yetu, kila mmoja wetu ana wajibu wa kupambana katika nafasi yake,"anaongeza Waziri Mpanda.

Mikakati iliyoainishwa na serikali kufanywa katika kupambana na malaria kupitia NMCP ni pamoja na kinga, kwa  kudhibiti wa mbu waenezao Malaria.

Utekelezaji wa mkakati huu unahusisha uboreshaji wa mazingira ili kuondoa mazalia ya mbu kwa kusafisha na kuboresha mifereji ya maji ya mvua, kuondoa madimbwi na kufanya usafi wa mazingira.

Anasema hatua hiyo linatekelezwa katika ngazi za Halmashauri pamoja na ushirikishaji wa jamii katika maeneo yao. 

Kwa kuzingatia Sheria mpya ya Afya ya Jamii ya Mwaka 2009, kila Kaya itawajibika katika kusimamia utekelezaji wa majukumu hayo na ufuatiliaji utafanywa na Halmashauri na kwa kupitia utekelezaji wa mpango huo maeneo mengi ya mazalio ya mbu yatadhibitiwa.

Waziri Mpanda anabainisha kuwa wizara inatekeleza mpango wa upuliziaji viatilifu ukoko kwenye kuta za ndani ya nyumba (IRS) ikilenga kwamba ifikapo mwaka 2013 iwe imefikia wilaya 60.

Mkakati huo umeanza katika mikoa ya Kagera, Mara na Mwanza ambapo jumla ya wilaya 18 zimefikiwa.

Maeneo yaliyofikiwa na mkakati huo kwa mafanikio ni Wilaya za Muleba na Karagwe na kwamba uwepo wa uambukizo na vifo vinavyotokea vimepungua kutoka asilimia 43 mwaka 2007 hadi chini ya asilimia 10 mwaka 2009.

Mkakati mwingine ni mpango wa kuua viluwiluwi, ambapo wizara imeanza kutekeleza mpango huo katika mazalio mbalimbali ya mbu na unagharamiwa na serikali kwa asilimia 100.

Anasema tayari mpango huo umeanza katika Jiji la Dar es Salaam ambapo kata zote jijini humo zitahusishwa na baadae kuendelea katika miji mingine.

Waziri Mpanda anasema sambamba na hilo serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Cuba zimekubaliana kujenga kiwanda cha kutengeneza viua viluwiluwi vya mbu.

Anasema mradi huo utaendeshwa katika wilaya ya Kibaha, Mkoani Pwani na kazi ya ujenzi wa kiwanda hicho inafanywa na wataalamu wa kampuni ya Labiofarm kutoka Cuba na inatarajiwa kukamilika mwaka  2012.

Matumizi sahihi ya vyandarua vyenye viuatilifu ni sehemu nyingine inayotiliwa mkazo na serikali kama mojawapo ya kinga dhidi ya maambukizi mapya ya malaria.

"Serikali imekuwa ikiendeleza na kuinua kiwango cha umiliki na matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu kwa muda mrefu (LLINs) majumbani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kugawa vyandarua.

Jumla ya vyandarua 9,034,677 viligawanywa kwa watoto chini ya miaka 5, Mwaka 2009 – 2010, pia chini ya mpango wa Hati Punguzo ya Watoto chini ya mwaka 1, vyandarua 2,040,260 vimetolewa,"anafafanua Waziri Mpanda.

Anasema kuwa wajawazito 4,675,347 walipata vyandarua chini ya Mpango wa Hati punguzo ya Tsh. 500/=.

Ili kukamilisha uwepo na matumizi ya vyandarua katika kila kaya kampeni ya ugawaji vyandarua sehemu za malazi katika kaya unahusisha nchi nzima na unatekelezwa kwa awamu.

Hadi mwishoni mwa mwezi Machi 2011 Kanda 5 zenye jumla ya mikoa 15 zimetekeleza hatua hiyo na vyandarua 10,656,293 vimegawiwa na hadi mwishoni mwa Mei mwaka huu ugawaji huo utakuwa umekamilika na jumla ya vyandarua 18,000,000 vitakuwa vimetolewa.

Waziri Mpanda anawataka wananchi kutumia  vyandarua hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhakikisha tatizo la malaria linapungua.

Utafiti unaonesha kuwa vyandarua hivi ni salama na madhubuti katika kupunguza tatizo la malaria kama kila mwananchi atalala kwenye chandarua kila siku.

Pamoja na mikakati ya kuhakikisha kuwa kinga dhidi ya maambukizi mapya inakuwa madhubuti, lakini pia serikali imezingatia tiba kwa wale watakaogundulika kuwa na vimelea vya malaria.

Kuangalia afya mara baada ya kuhisi dalili za homa ni muhimu, hasa kwa watoto wadogo kwani utafiti unaonesha kuwa watoto 6 kati ya 10 wenye homa hucheleweshwa matibabu kwa zaidi ya siku moja tangu homa kuanza.

Anasema hiyo ni moja ya sababu kubwa inayochangia vifo vya watoto wanaougua malaria nchini.

"Wito wangu kwa wananchi wote ni kuwaomba wawapeleke mapema watoto kwenye vituo vya tiba mara tu wanapoanza kuona dalili za ugonjwa.

Kamilisheni matibabu ambayo mgonjwa ameshauriwa na wataalamu wa afya. Jukumu la serikali ni kuhakikisha kuwa dawa na vifaa tiba vinapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma za tiba,"anasisitiza Waziri Mponda.

Katika jitihada za kupambana na ugonjwa wa malaria, vituo vyote vya umma vya kutoa huduma za Afya nchini (Tanzania Bara) vilianza kutoa matibabu ya malaria kwa kutumia dawa mseto kuanzia Disemba moja  2006.

Dawa hizo zimekuwa zikipatikana kwa kiasi cha Shilingi 500 katika hospitali za umma wakati katika vituo binafsi na maduka ya dawa zilikuwa zikipatikana kwa gharama kati ya shilingi 10,000 hadi shilingi  15,000 kwa dozi moja.

Katika hilo Waziri Mpanda anasema kuwa tayari serikali kupitia wizara yake imehakikisha dawa mseto za kutibu malaria zinapatikana katika vituo binafsi vya afya na maduka ya dawa kwa bei moja ya punguzo.

"Hii itawezesha wananchi kuelewa kuwa dawa hizo tayari zimeishalipiwa na serikali sehemu kubwa na mwananchi anatakiwa asiinunue kwa zaidi ya shilingi 1000.

Iwapo kuna maduka yatakayokuwa yanauza dawa hiyo zaidi ya kiwango hicho taarifa zitolewe kwa vyombo husika ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa mapema dhidi ya mmiliki na muuzaji wa dawa hiyo,"anatoa angalizo Waziri Mpanda.

Uchunguzi wa ugonjwa wa malaria kutumia vipimo vya maabara pia umeboreshwa ambapo serikali imeanza kusambaza katika vituo vya afya kipimo cha malaria kinachotoa majibu haraka kinachoitwa ‘Rapid Diagnostic Tests for Malaria’.

Anasema kipimo hicho kitasaidia huduma za uchunguzi za ugonjwa wa malaria zitolewazo na hadubini na lengo likiwa ni kuongeza uhakika wa ainisho la ugonjwa wa malaria kwa wagonjwa wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huo ili kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima ya dawa za kutibu malaria.

Kwa upande wa wajawazito Waziri Mpanda anasema si Hati Punguzo pekee wanazopata kina mama, bali pia serikali huwapatia tiba ya tahadhari pale mjamzito anapoenda kliniki kwa awamu mbili katika kipindi cha ujauzito.

Ushiriki wa jamii katika mikakati ya kudhibiti malaria ni muhimu ili kupata mafanikio dhahiri, na waziri anazitaka Halmashauri zote kuweka bajeti ya kudhibiti malaria katika Mipango yao Kamambe ya Afya (CCHPs).

Anawataja wahisani wakubwa wanaosaidia katika mapambano dhidi ya Malaria kuwa ni pamoja na Mfuko wa Dunia wa kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund for HIV/AIDS, TB and Malaria).

Anataja Mpango Maalum wa Rais wa Marekani wa kupambana na Malaria (PMI) na Benki ya Dunia (WB), Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Kimataifa la Kuhudhumia Watoto (UNICEF) kuwa ni wadau wakubwa wanaosdia nchi katika suala la maleria.

Antaja wengine kuwa ni Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Kituo cha Utafiti cha Ifakara (IHI), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi za Tiba Muhimbili (MUHAS) na Shirika la Afya Bugando.

No comments:

Post a Comment