Na Benjamin Masese
APRILI 4 mwaka huu ilikuwa ni siku muhimu iliyokuwa ikisubiriwa na wafanyakazi wa kampuni ya Reli Tanzania (TRL).Siku hiyo ilikuwa ni siku ya mkutano wao uliokuwa umeitishwa na
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi (TRAWU)Bw. Slyvester Rwegasira, aambaye sasa ni marehemu.
Kabla ya saa za mkutano kutimia na kujikusanya katika ukumbi wao maarufu kama Kapuya ghafla Bw. Rwegasira alipatwa na mauti siku hiyo hiyo katika hospitali ya Dar Group kutokana shinikizo la damu.
Tukio hilo ilimshtua kila mtu anayemfahamu marehemu Rwegasiara hasa wafanyakazi wa TRL ambao walikuwa wakimwona kama mungu wao wa pili baada Mungu Mkuu muumba Mbingu na Nchi.
Haikuwa rahisi kuamini mpambanaji kama yule mwenye afya nzuri na mwenye msimamo katika kusimamia haki za wafanyakazi katoweka ghafla duniani huku akiwa na ujumbe mzito moyoni ya hatma ya wafanyakazi wa TRL.
Baada ya siku kumi kupita uliitishwa mkutano wa kwanza na Mwenyekiti wa TRAWU Taifa Bw. Bakari Kiswala, uliokuwa na mada nne.
Mada hizo ni kudai rasmi kifuta jasho, kumuombea dua marehemu Rwegasira na maandalizi ya kuziba nafasi hiyo pamoja na kupinga kauli inayotolewa na Waziri wa Uchukuzi Bw. Omara Nundu kwa Rais Jakaya Kikwete kwamba wafanyakazi wa TRL ni wakorofi na hawatawaliki.
Bw. Kiswala anasema Shirika la Reli Tanzania (Tanzania Railways Corporation-TRC) lilianzishwa mwaka 1977 kwa sheria namba 11 ya mwaka huo kutokana na kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Anasema wakati EAC inavunjika wafanyakazi wa TRC walikuwa chini ya East African Railways and Harbours (EARc).
Anasema mwaka 2000 taarifa ya kusudio la serikali kutaka kubinafsisha shirika hilo ilitolewa na menejimenti kwa kuwapa TRAWU nakala ya ripoti ya mapendekezo ya kupunguza wafanyakazi.
Anasema hatua hiyo ilifikiwa katika kikao kilichofanyika siku tatu Msimbazi Center-Dar es Salaam kuanzia Mei 25 hadi 27 mwaka 2000.
Anasema Aprili 30, 2002 na Mei 1,2002 ulifanyika mkutano mkubwa wa pamoja baina ya TRAWU na Menejimenti ya shirika la Reli Tanzania na wawakilishi wa serikali katika ukumbi wa PPF House-Dar es Salaam kujadili upunguzaji wafanyakazi.
Anasema kwa upande wa serikali iliwakilishwa na Tume ya Rais ya kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC), Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha na Tume ya Mipango.
Anasema katika kikao hicho serikali ilikubali kuwa wafanyakazi wote watalipwa mafao hata wale watakaochukuliwa na mkodishaji (mwekezaji) isipokuwa wale watakaobaki TRC-Mfilisi (TRC-Residual na wale wa Railways Assets Holding Company (RAHCO).
Anasema serikali ilitoa taarifa kwamba ilishakwisha fanya utafiti kuhusu mashirika yote yanayobinafsishwa na kuona mafao ya wafanyakazi ni mzigo mkubwa kwao na kupendekeza kuwa mafao yasiyo ya kisheria hayatakuwa miongoni mwa malipo yatakayofanywa na serikali.
Bw. Kiswala anansema kutokana na kauli hiyo ya serikali TRAWU iliwaomba wafanyakazi watakaohamishiwa RAHCO na TRC ya muda nao wahusike kulipwa mafao yao.
Hata hivyo serikali ilisisitiza kuwa sheria ya reli ya mwaka 2002 iliyopitishwa na bunge inawataka wasilipwe kwa sababu idadi yao ilikuwa ndogo isiyofikiwa wafanyakazi 100.
Serikali ilisema kutokana na maelezo ya sheria wafanyakazi watakaoendelea na utumishi hadi watakapofikia umri wa kustafu lakini TRAWU haikukubaliana na maelezo hayo na kutaka kulipwa mafao yao kisheria.
Anasema hapo ndipo suala la mkono wa heri lilipoibuka ambapo serikali ililazimika kuunda Kamati ya Baraza la Mawaziri na watalaam ambalo lilikutana na TRAWU kujadili kwa kina suala hilo na mkataba wa hiari yaani kuendelea kufanya kazi na mwekezaji.
Anasema baada ya majadiliano marefu ilikubaliwa kuwa wafanyakazi watakaopunguzwa ndio watakaolipwa mkono wa heri.
Upande wa TRAWU walipendekeza kupunguzwa wote ikiwa lengo lao ni kutaka kuondokana na usumbufu kutoka kwa mwajiri mpya na pia nwaliona ni njia pekee ya kuanza mkataba mpya na mwekezaji atakayepatina.
Anasema serikali iliendelea kushikilia msimamo wao ambapo TRAWU iliona suala la kupunguzwa wafanyakazi haliwezekani kutokana na uwezo, unyeti wa shughuli za kazi yenyewe lakini bado wafanyakazi walipenda kuanza mkataba mpya na mwajiri hasa wale waliotoka EARC kwenda TRC na hatimaye kuchukuliwa na sekta binafsi yaani RITES ya India.
Kwa nini wafanyakazi walipwe
Anasema zipo sababu kuu sita zinazofanya wafanyakazi kudai kulipwa kifuta jasho ikiwa ni pamoia na mabadiliko ya uendeshaji wa shirika kutoka TRC kwenda TRL yaliyofanyika mwaka 2007 baada kubinafsishwa kwa (RITES).
Pili kutokana na hali ilitakiwa wafanyakazi walipwe wote lakini kinyume chake walilipwa wale tu walioachishwa kazi huku serikali ikiwapa matumaini kwamba mara baada ya mwekezaji kupatikana watahakikisha anabaoresha zaidi hali za kimaisha za wafanyakazi lakini hali ni tofauti.
tatu, stahili za kisheria kama vile Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na PPF zimeendelea kuwa ndogo kwani kanuni za malipo ya mifuko hiyo haimruhusu mfanyakazi wa TRL kukopa kwa sababu hawana mwajiri kamili.
Nne, vigezo vilivyotumika katika kuendelea na kazi kutoka TRC hadi TRL ilikuwa ni utumishi bora, uaminifu, uadilifu lakini mwekezaji RITES alishindwa kuzingatiwa vigezo hivyo huku akilipa mafao kidogo ukilinganishwa na mfanyakazi aliyeachiwa kazi mwaka 2007.
Anasema awali mwajiri alikuwa akilipa mfanyakazi mstaafu malipo ya severance, lakini mwaka 2010 ilifanya mabadiliko na kufuta kabisa malipo hayo.
Anatoa mfano kwa mfanyakazi aliyeajiriwa mwaka 1968 na kustaafu 2010 analipwa kiinua mgongo cha sh. 1.221,546.70 kwa mshahara wa sh.523,520 kwa mwezi.
Tano, anasema mwajiri wa TRL amesababisha mazingira ya kazi kuwa magumu na kutovumilika kiasi cha kufanya malengo na matarajio ya kampuni kutofikiwa toka alipoanza rasmi uendeshaji mwaka 2007.
Anataja baadhi kuwa ni kutozingatia uwepo wa vitendea kazi, kujali rasilimali watu, mazingira mazuri ya kazi kama ofisi, karakana na kutokuwepo na dhamana ya mfanyakazi kukopa katika taasisi za fedha.
Mwisho anasema ili kutoa ushirikiano katika kuendesha kampuni na kujenga morali na moyo wa kujituma zaidi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku serikali inabidi iwalipe wafanyakazi kifuta jasho tofauti na hapo isitegemee maendeleo ya reli.
Mapendekezo ya namna ya kulipwa
Anasema wafanyakazi wanapendekeza malipo yao yafanyike kwa kuzingatia kiwango cha mshahara na daraja lake ili kuleta uwiano usio na tofauti kubwa baina ya wafanyakazi wa daraja la juu na chini.
Anasema wafanyakazi wanatakiwa kupewa mshahara wa miezi iliyopendekeza kwa kuzingatia kima cha mishahara ya mwezi Januari 2011 kama vilivyotumika mwaka 2007 wakati wa kumaliza mkataba na iliyokuwa Tanzania Railways Corporation (TRC) kwenda
Daraja la kima cha chini kabisa ( TRD 1) sh. 200,000 hadi TRD 6 wapewe mishahara (basic salary ) ya miezi 40, TRC 1 hadi TRC 6 miezi 35, TRB 1 hadi TRB 3 miezi 35, TRB 4 hadi TRB 6 miezi 30 na TRA 1 hadi TRA 5 miezi 20.(kima cha juu)
Anasema pamoja na kuwa viwango vya mishahara ya mwaka 2007 vilikuwa tofauti lakini inapendekezwa kutumia viwango vya sasa kutokana na kushuka kwa thamani ya pesa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei kati ya mwaka 2007 na 2011.
No comments:
Post a Comment