tangazo

Thursday, May 5, 2011

Waziri Ghasia: Tutamaliza kero ya watumishi hewa serikalini

*Rais Kikwete: Warasimu wasivumiliwe kamwe

Na John Daniel

MOJAWAPO ya kilio cha watanzania ni serikali kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma katika sekta mbalimbali kinyume cha sheria.Mojawapo ya eneo inayolalamikiwa zaidi kwa
uzembe wa wazi ni malipo ya mishahara kwa watumishi hewa.

Kilio hiki ni cha muda mrefu na karibu kila awamu imekuwa ikijaribu kupambana na tatizo hilo lakini bila mafanikio.Swali kubwa kwa watanzania ni je nani anayewajibika kuhakiki na kujua idadi halisi ya watumishi wa umma ili kumaliza tatuzi hlo hasa kwa kuzingatia kuwa nchi yetu bado ni changa kiuchumi hivyo kuhitajika juhudi kubwa zaidi kutunza kidogo kilichopo.

Ili kufikia lengo Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Hawa Ghasia, anaelezea jinsi Wizara yake ilivyopambana na kunua kumaliza kabisa tatizo hilo.

Waziri Ghasia anaweka wazi kuwa jumla ya shilingi bilioni 9.2 zimepotea kwa kulipa mishahara watumishi hewa kuanzia mwaka 2007 hadi 2009.

Anasema Fedha hizo zililipwa katika sekta tatu muhimu za elimu, afya na Mahakama.

Anasema yeye kama Waziri pia aliguswa na tatizo hilo la matumizi mabaya ya fedha za umma na kuanza uhakiki wa watumishi wote halali.

Anafafanua kuwa uhakiki huo unalenga kumaliza tatizo hilo ma kupunguza matumizi mabaya ya fedha za umma huku nchi ikiendelea kukabiliwa na upungufu wa wataalam katika kada mbalimbali.


Anasema watumishi hewa 1,413 waligundulika katika sekta ya elimu na malipo ya shilingi 3,043,609,700 huku watumishi 1,511 na malipo shilingi 4,482,992,570 zikigundulika katika sekta ya afya.

Kwa upande wa sekta ya mahakama Waziri Ghasia anasema jumla ya watumishi 423 na malipo ya hewa ya shilingi 1,686,726,710 ziligundulika.

"Zoezi hili linaendelea katika sekta ya kilimo,mifugo na Uvuvi,"anasema Waziri Ghasia.

Anasema ili kumaliza kabisa tatizo hilo Wizara yake imebuni mfumo mpya maalum wa kisasa wa kutunza takwimu zote za watumishi wa umma.

Anasema mtumishi akifariki, kuacha kazi, kufukuzwa au kustaafu malipo yake yanasimishwa mara moja bila kutumia ujanja.

Anasema katika uhakiki huo Wizara yake ilibaini kwamba baadhi ya watumishi wa umma hawana taarifa sahihi za kiutumishi na mishahara.

Anasema kutopandishwa vyeo na kutochukuliwa hatua za kinidhamu kwa wakati kwa watumishi wanaokiuka madili ya kuhudumia umma nalo ni tatizo waliyobaini katika utekelezaji wa uhakiki huo.

Anataja hatua za haraka zilizochukuliwa kumaliza matatizo hayo kuwa ni pamoja na kuwafuta watumishi hewa 3,347 kwenye orodha ya malipo ya mihahara.

Hataua nyingine ni kuwasiliana na Idara na vyombo husika vya dola kushughulikia wahusika walioisababishaia serikali hasara ya fedha hizo.

Anasema Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na ofisi ya Taifa ya ukaguzi ndio waliokabidhiwa jukumu kubaini watu waliohusika katika njama hizo.

Anasema Ofisi yake imewaagiza waajiri wote kutoa kipaumbele katika kusimamia masuala ya rasilimali watu na udhibiti wa orodha ya mishahara pamoja na kuimarisha mfumo wa malipo ya mishahara ili kuondoka mianya watumishi hewa.
                                 
"Pia tumeanzisha tovuti kuu ya Serikali ambayo itatumia kutoa huduma kwa nia ya mtandao. Tovuti hii itarahisisha utoaji huduma kwa wananchi.

"Wananchi wataweza kupata huduma bila kulazimika kutembelea hadi ofisi husika. Tovuti hii ipo katika majaribio kabla ya kuanza kutumika rasmi mwezi Juni, 2011,"anasema Waziri Ghasia.

Anasema ili kupima matokeo ya utekeleza wa majukumu yao kama Wizara inayowajibika na utumishi wa umma kwa ujumla walianzisha mpango wa kufanyiwa tathmini ili kujua kama wamefikia hatu inayotakiwa au la.

Anasema hatua hiyo inazingatia msingi na programu ya kuleta mabadiliko ya utendaji kazi katika utumishi wa umma na kwamba wanatumia utaratibu wa kufanya tathmini huru kuona kama tunapata matokeo tarajiwa kwa walengwa ambao ni wananchi.

Anafafanua kuwa katika tathmini ya kwanza iliyohusu matokeo yanayotokana na mifumo ya kimenejimenti iliyowekwa chini ya programu hiyo mwaka 2010 ilionyesha kuwa wanatoa huduma bora.

Anataja baadhi ya vigezo vilivyotumika kuwapima kuwa ni matumizi ya mipango mkakati, Upimaji Utendaji wa kazi kwa njia ya Uwazi  (OPRAS) na matumizi ya mikataba ya huduma kwa wateja.

"Tathimini hii ilifanywa na Kampuni ya TECHTOP CONSULT TANZANIA LTD na matokeo yalionesha kuwa asilimia 62 ya taasisi za umma zilikuwa zinatumia mifumo hiyo katika kutoa huduma bora kwa wateja wake,"anasema.

Ataja Wizara zilizofanya vizuri katika tathimini hiyo kuwa ni Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Viwanda na Biashara, Kilimo,Chakula na Ushirika.

Nyingine ni Kazi na Ajira,Maji na Umwagiliaji, Maendeleo ya Jamii,Jinsi na Watoto, Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Nishati na Madini pamoja na MiundoMbinu.

Anasema tathimini ya pili ilifanyika kupima namna Wizara yake inavyotekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa katika Hati ya Rais ya mgawanyo wa majukumu ya kuanzishwa kwake.

"Tathimini hii ambayo ilifanywa na Kampuni ya PRICEWATERHOUSE COOPERS (PWC) ilihusisha  mahojiano na watumishi wa umma 400 na ililenga kubainisha endapo walikuwa wanaridhika na kiwango cha huduma zinazotolewa na Ofisi hii.

Asilimia 80 ya watumishi hao walionyesha kuridhishwa na utekelezaji wa majukumu yetu kama wasimamizi wa sekta ya Utumishi wa umma,"anasema.

Anasema tathimini ya tatu iliyohusu utoaji  taarifa za Serikali kwa wanaozihitaji  iliyofanywa na Kampuni ya KIM CONSULTING LTD nayo ilionyesha kuwa asilimia 75 ya waliohojiwa katika tathimini hiyo walionesha kuridhishwa na kiwango cha upatikanaji wa taarifa kutoka Serikalini.

Anasema utafiti uliofanywa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) pia ulionyesha kuwa wanatoa huduma bora na walikabidhiwa tuzo kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa uwazi zaidi.

Anasema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma inashirikiana kwa karibu na Idara mbili zinazojitokeza katika kutekeleza majukumu yake ambazo ni Tume ya Utumishi wa Umma na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Anasema Tume ya Utumishi wa Umma imeundwa kwa mujibu wa kifungu amba 9 (1) cha Sheria ya utumishi wa umma namba 8 ya mwaka 2002 kama na marekebisho yake chini ya Sheria namba 18 ya mwaka 2007.

Anasema tume hiyo inaongozwa na Mwenyekiti na Makamishna sita huku Sekretarieti ya tume ikiongozwa na Katibu na kwamba ina Idara nne, Divisheni moja na vitengo sita pamoja na  Ofisi za Idara ya Utumishi wa Walimu katika mikoa na wilaya zote Tanzania  Bara.

Anataja wajibu wa tume kuwa ni kuhakikisha  kuwa masuala ya rasilimaliwatu katika Utumishi wa umma yanaendeshwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu kwa lengo la kuimarisha utendaji unaozingatia malengo na matokeo yanayopimika.

"Tume ni Mamlaka ya Rufaa kwa watumishi wa umma dhidi ya maamuzi yanayotolewa na mamlaka zao za nidhamu,"anasema.

Anasema ili kuhakikisha masuala ya rasilimaliwatu katika Utumishi wa umma yanaendeshwa kwa kuzingatia Sheria Kanuni na Taratibu mbalimbali wamebuni mbinu mpya.

Anataja mbinu hizo kuwa ni pamoja na kusafisha taarifa za watumishi (Data Cleaning) kazi ambayo utekelezaji wake ulianza mwezi Desemba mwaka jana.

Anafafanua kuwa hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu jumla ya Wizara nane, Idara tano zinazojitegemea, Secretarieti za mikoa 14 na Mamlaka za serikali za mitaa 16 tayari zimekamilisha utaratibu huo.

"Faida ya zoezi hilo ni pamoja na kuondoa uwezekano wa kuwepo watumishi hewa katika orodha ya malipo ya mishahara, kuwepo kwa kumbukumbu sahihi za watumishi pamoja na kuondoa uwezekano wa watumishi kulipwa mishahara isiyolingana na vyeo vyao,"anasema.

Kero ya watumishi wapya

Waziri Ghasia anasema licha ya kuwepo kwa malipo hewa pia kero nyingine kubwa kwa watumishi wa umma ni kufanya kazi bila mishahara kwa muda mrefu kinyume cha sheria, taratibu na kanuni.

Anasema jambo hilo husababisha huduma hafifu kwa wananchi kwa kuwa watumishi husika wanaona hawana thamani.

"Ili kumaliza tatizo hilo Wizara imeanzisha Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (Human Capital Management and Information System-HCMIS).

"Chini ya Mfumo huu watumishi wapya wanaweza kuingizwa kwenye orodha ya malipo ya mishahara muda mfupi baada ya kuajiriwa na kuripoti katika vituo vyao vya kazi,"anasema.

Anasema kumbukumbu zote za mwajiri huingizwa kwenye kompyuta mara tu baada ya kupewa barua ya jira na akiripoti tu anaingizwa kwenye mfumo wa malipo bila kuchelewa.

Anasema jambo hilo linawezekana kwa kuwa watumishi wote wa umma wanapewa ajira baada ya bajeti hivyo hakuna sababu ya mshahara wa mtumishi kuchelewa kutokana na uzembe wa watu wachache.

"Mfumo huu umeanza kutumika na kuonyesha mafanikio katika Halmashauri za Wilaya 25 za mikoa ya Tabora, Kigoma,Mbeya,Mtwara, Pwani, Mwanza,Mara na Arusha,"anasema Bi. Ghasia.

Anasema Wizara yake imepanga kuhakikisha mfumo huo unawekwa katika Wizara zote, Idara zinazojitegemea na Mamlaka zote za Serikali za Mitaa ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.

Kuhusu juhudi za kuunganisha serikali kwa mtandao mmoja anasema hadi sasa Wizara yake imefanikiwa kuunganisha Ofisi yake,Tume ya Mipango,Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, afya na Ustawi wa Jamii, Ofisi za Bunge na kituo cha mafunzo kwa njia ya mtandao katika mawasiliano
ya serikali.
                                 
"Pia tumeanzisha tovuti kuu ya Serikali ambayo itatumia kutoa huduma kwa njia ya mtandao, lengo kuu ni kuboresha huduma kwa wananchi wetu.

Tovuti hii itarahisisha utoaaji huduma kwa wananchi kwa kuwawezesha kupata huduma bila kulazimika kutembelea ofisi husika. Tovuti hii ipo katika majaribio kabla ya kuanza kutumika rasmi mwezi Juni, 2011,"anasema.

Anataja baadhi ya majukumu ya Tume ya Utumishi wa umma kuwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa kawaida kwa taasisi za umma 194, ukaguzi maalum kufuatilia malalamiko ya watumishi katika taasisi za umma 40.

Anasema ili kumaliza tatizo la ajira katika sekta ya umma Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma imeanzishwa rasmi katika mwaka wa fedha 2009/2010 kama chombo kipya cha kushughulikia mchakato wa ajira.

Anasema chombo hicho kitasaidia kutafuta wataalamu wenye ujuzi na kuandaa mfumo wa kuhifadhi taarifa za wataalam hao ili kurahisisha utaratibu wa ajira.

Anasema pia itandaa orodha ya wahitimu wa vyuo vikuu na wataalam weledi kwa madhumuni ya kurahisisha rejea na ujazaji nafasi wazi za ajira katika utumishi wa umma, kutangaza nafasi wazi za kazi zinzotokea katika utumishi wa umma na kuwashauri waajiri kuhusiana na masuala ya ajira.

Anasema sekretarieti ya ajira imetekeleza mambo mbalimbali ikiwemo kutangaza na kuendesha usaili kwa waombaji kazi 19,190 ili kujaza nafasi 1,558 zilizotangazwa za waajiri 82 ambapo nafasi 1,498 zilijazwa.

Anasema nafasi 60 hazikupata waombaji wenye sifa na kutangazwa upya na kwamba Sekretarieti hiyo imeandaa mpango mkakati na kuuwasilisha kwa wadau kuainisha mahitaji ya kazi za watumishi pamoja na kutembelea waajiri na wadau kwa ajili ya kujitambulisha na kuandaa mfumo wa awali wa uendeshaji mchakato wa ajira kabla ya kuweka mfumo thebiti wenye kutumia TEKNOHAMA usiorushu upendeleo katika kuendesha mchakato wa ajira.

Kwa upande wake Rais Jakaya Kikwete anasema licha ya kazi kubwa inayofanywa na Wziara hiyo lakini tatizo la urasimu bado lipo serikali na kwamba anataka tiba kamili ya tatizo hilo.

Anasema inampa wasiwasi kama bado watumishi wa umma wanaweza kupata uhamisho na kuteseka kwa kukosa malipo ya likizo wakati serikali inapanga bajeti yake kabla ya kutekeleza.

"Urasimu bado upo serikalini na hii inanipa tabu sana, watu wananiambia, sasa shughulikieni hawa wachache wanaotuharibia haya mambo mazuri kiasi hiki.

Lakini pia msihaamishe mtumishi kama hakuna fungu la fedha kumlipa maana mnaweza kutesa watu,"anasema Rais Kikwete.

Kuhusu kupandisha vyeo watumishi anasema bado anaumia na malalamiko ya watumishi wa umma kuhusu kupandishwa vyeo hususan walimu.

"Kama mtu hataki kupandisha walio chini yake nyie utumishi mpandisheni, na mhakikishe mnamshughulikia huyo mrasimu, mkishindwa nileteenia Katibu Mkuu Kiongozi atawashughulikia, hatuwezi kuvumilia hihco,"anasema Rais Kikwete.

Anasema wajibu mkubwa wa watumishi wa umma ni kuhudumia wananchi na kwamba lengo hilo haliwezi kufikiwa kama watumishi hao hawaoati haki zao kwa sababu ya watu fulani.

"Kwa kweli nawapongezi sana Wizara hii, mmejitahidi sana na mmefika mbali,muendelee mimi nitawaunga mkono,"anamaliza Rais Kikwete.

No comments:

Post a Comment